Mshambuliaji Erling Haaland alivaa kiatu maalumu kilichotengenezwa kwa ajili yake baada ya kuvunja rekodi ya upachikaji wa mabao Ligi Kuu England kwa msimu 2022/23, lakini akalizimika kubadilisha baada ya kufunga dhidi ya Everton mwishoni mwa juma lililopita.

Mshambuliaji huyo alivaa kiatu kilichotengenezwa na Nike kikiwa kimeandikwa mabao 35 aliyofunga na kuvunja rekodi.

Hata hivyo, Haaland akaongeza idadi ya mabao kwa kupachika la 36 dhidi ya Everton katika mechi ya Ligi Kuu England.

Kabla ya mchezo huo Haaland alivunja rekodi katika mchezo mwingine wa ligi dhidi ya West Ham United katika ushindi wa mabao 3-0 uliochezwa mwezi huu.

Baada ya mchezo kumalizika mchezaji huyo aliweka picha ya kiatu chake kwenye akaunti yake ya Instagram mara tu kiliporekebishwa namba kwani awali iliandikwa idadi ya mabao 35, ambapo namba tano ilifutwa na kuandikwa sita kwa kutumia kalamu baada ya kufunga bao la 36.

Kutokana na uwezo wake wa upachikaji mabao Haaland anahitaji zaidi kiatu kingine kilichotengenezwa maalumu kila anapoongeza idadi ya mabao kabla ya msimu kumalizika.

Man City imebakiza mechi tatu za ligi huku ikikaribia ubingwa wa Ligi Kuu ya England kwa mara ya tatu mfululizo.

Vilevile Man City ilishatinga Fainali ya Kombe la FA na pia itacheza mechi ya marudiano ya Nusu Fainali ya Ligi Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Real Madrid kesho Jumatano (Mei 17), katika Uwanja wa Etihad. Mchezo wa kwanza timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Nani kusonga Fainali UCL leo City, Madrid, Inter na Milan
Bosi Chelsea ajuta kumfuta kazi Tuchel