Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejipanga kukamilisha uandaaji wa mitaala itakayoendana na mahitaji ya sasa na kuwezesha wahitimu kuwa na ujuzi na maarifa stahiki, huku ikitaka kipaumbele kiwe kwenye elimu ya ufundi na kuongeza idadi ya walimu ili kukabiliana na upungufu..
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma na kuliomba Bunge kuidhinisha kiasi cha Shilingi 1.7 trilioni kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mambo mbalimbali, ikiwemo kuboresha mitaala katika mwaka wa fedha 2023/24.
Amesema, kati ya kiasi alichoomba kiidhinishwe, Shilingi 537.9 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida wakati Shilingi 500.957 bilioni zitatumika kwa ajili ya mishahara huku kiasi cha Shilingi 36.9 bilioni kikiwa ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Aidha Prof. Mkenda ameongeza kuwa kiasi hicho cha fedha kinachoombwa kuidhinishwa ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo Shilingi 979.08 bilioni ni fedha za ndani na Shilingi 158.8 bilioni ni fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo.