Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema itaendelea kusisitiza uwepo wa ligi za mpira wa miguu zenye ubora katika maeneo ya mijini na vijijini, lengo likiwa kukuza viwango vya wachezaji.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Tabia Maulid Mwita, wakati akijibu swali la Abdallah Abasi Wadi, Mwakilishi wa Jimbo la Nungwi, ambaye alitaka kujua jitihada ambazo zimechukuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) na Chama cha Netiboli Zanzibar (CHANEZA) katika kukuza vipaji.
Akijibu swali hilo, Tabia amesema wizara yake inatambua umuhimu wa kuwepo kwa vipaji vya michezo mbalimbali katika maeneo ya mijini na vijijini na ndio maana inasisitiza kuwepo kwa ligi zenye ubora katika ngazi mbalimbali.
“Kwa kuwa klabu za mpira wa miguu zipo hadi vijijini na huko ndiko vipaji vingi vinavyopatikana, kama ZFF na CHÁNEZA zitavifuatilia na kuvitambua vipaji tutapata wachezaji bora zaidi wa timu za Taifa,” alisema
Amesema ZFF imehamasisha na kuongeza ushindani wa ligi katika ngazi zote kuanzia Ligi Kuu ya Zanzibar hadi Ligi Daraja la Tatu.
Pia, waziri huyo alisema kwa upande wa CHANEZA, inatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi wa ngazí za wilaya katika Visiwa vya Unguja na Pemba na jukumu kubwa litakuwa kukuza mchezo huo katika ngazi za chini.