Mabosi wa Ligi Kuu England watakwenda Etihad Jumapili ijayo kuwakabidhi Manchester City taji la Ligi Kuu England – endapo watashinda.
Ushindi dhidi ya Chelsea siku hiyo utatosha kuipa Man City taji la tano la Ligi Kuu England katika kipindi cha misimu sita.
Man City inaweza kubeba ubingwa bila kuifunga Chelsea Jumapili huko Etihad kama Arsenal watapigwa na Nottingham Forest, Jumamosi. Man City itahitaji alama moja kama Arsenal itatoka sare na Forest wanaopambana wasishuke.
Mechi ya Jumapili itakuwa ya mwisho kwa Man City kuwa nyumbani msimu huu, hivyo kocha Pep Guardiola na jeshi lake watapewa taji baada ya mechi kama watashinda.
Hiyo ina maana ni shughuli pevu kwa bosi wa Ligi Kuu England, Richard Masters kutokana na kile alichofichua kuhusu Man City kufanya makosa 115 yanayohusu udhibiti wa Ligi Kuu England.
Bado hakuna uhakika wa kamati ya tume huru kama itafanikisha jambo hilo kwa haraka na huenda likachukua miezi kadhaa kupata ufumbuzi wa shutuma zinazoikabili Man City katika ukiukwaji wa mambo kibao ya kanuni za udhibiti kwenye Ligi Kuu.
Kama Arsenal inashinda na kisha Man City ikashindwa dhidi ya Chelsea, basi sherehe za kukabidhi kombe zitasubiri hadi siku ya mwisho ya msimu, Mei 28, ambapo katika mechi hiyo, Man City watakuwa ugenini kukipiga na Brentford.