Baada ya kutinga hatua ya Fainali ya mashindano ya Kombe la shirikisho ‘ASFC’, Uongozi wa Azam FC umesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na kumaliza msimu huu wakiwa wameshinda taji hilo.

Azam FC itacheza fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa kukutana na mshindi kati ya Young Africans na Singida Big Stars ambao wanakutana Jumapili kwenye Uwanja wa CCM Liti ulioko Singida.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2013/14 wamesonga mbele katika mashindano hayo kwa kuifunga Simba mabao 2-1 Matajiri hao wa Chamazi walipotea mapema katika mbio ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na kutolewa pia kwenye michuano ya kimataifa hatua za awali.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema wanaimani na kikosi chao itafanya vizuri katika mchezo huo wa fainali na wako tayari kukutana na timu yoyote kati ya Singida Big Stars au Young Africans.

Popat amesema baada ya kutofikia malengo ya kutwaa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambalo limechukuliwa na Young Africans, matumaini yao yameeleka katika kulinyakua Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.

“Tumejipanga vizuri na tayari tumeongeza nguvu kwenye benchi la ufundi kwa kumleta, Youssouph Dabo, ambaye ndiye kocha wetu kwa sasa, tuna matumaini makubwa kutoka kwake, pia wachezaji wanahitaji fainali hiyo,” amesema Popat.

Katika Michuano hiyo Young Africans ndio mabingwa watetezi wa ambayo bingwa wake anakwenda katika michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Young Africans yajinadi kuimarika 2023/24
Dkt. Musa ataka migogoro vyama vya ushirika itatuliwe