Uongozi wa Klabu ya Ruvu Shooting umewaangukia mashabiki na kuwaomba radhi kufuatia timu hiyo kushuka daraja msimu huu 2022/23.
Msemaji wa klabu hiyo, Masau Bwire, amesema kushuka daraja kwa timu hiyo kumewaumiza na kuwaomba radhi mashabiki wa timu hiyo ambao wamekuwa wakiisapoti muda wote.
Bwire ameweka wazi kuwa wadau wengi wa mpira wa miguu nchini walitamani timu hiyo iendelee kushiriki kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara huku wakitarajia makubwa msimu ujao.
“Kwanza ninawaomba radhi wapenzi wa Ruvu Shooting na Watanzania kwa sisi kushuka daraja, naamini wengi wao walikuwa wanatamani kuona timu yetu inaendelea msimu ujao,” amesema Bwire.
Amesema amepokea kwa mikono miwili kile kilichowakumba msimu huu na kudai wanakwenda kuiamsha Ligi daraja la kwanza ambayo kwa sasa imepoteza msisimko.
“Tunajiandaa na ligi daraja la kwanza ambayo imepoteza msisimko, tunataka tuwaonyeshe sisi ni nani ili msimu ujao turudi tunakostahili kuwapo, yaani kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara,” amesema Bwire.
Aidha amesema baada ya kumaliza michezo yao miwili iliyobakia msimu huu moja kwa moja wataanza maandalizi ya Ligi daraja la kwanza.
“Tunaomba mashabiki pamoja na wadau wetu waendelee kutupa ushirikiano kwani naamini tutarejea kwenye ligi na tutarejea kwa kishindo,” amesema msemaji huyo.