Rais wa Klabu ya Young Africans Injinia Hersi Said amesema msimamo wa klabu dhidi ya Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ bado upo vilevile na hautabadilika.
Young Africans na Feisal Salum wapo katika mgogoro wa kimkataba, huku kiungo huyo akishinikiza mkataba wake kuvunjwa kupitia TFF, lakini Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeamuru suala hilo haliwezekani, zaidi ya pande hizo mbili kukaa mezani na kumalizana.
Akizungumza mapema leo Jumatano (Mei 24) kupitia Clouds FM Injinia Hersi Said amesema, Young Africans ni Taasisi na haiwezi kuwa na huruma katika suala hilo, zaidi ya kusimamia misingi iliyojiwekea.
Amesema tayari Klabu imeshatangaza njia tatu ambazo ni sahihi kwa mchezaji Feisal kumaliza sakata lake, ambazo wanaamini zikifuatwa hakutakuwa na maneno maneno yanayoendelea katika Mitandao ya Kijamii na baadhi ya vyombo vya Habari.
“Young Africans ni Taasisi, na Taasisi haisikii huruma kwa mtu, Feisal Salum tumempa Option tatu, Moja anatakiwa kuja kuutumikia mkataba wake na Yanga, Pili aje tujadili kuusu kuboreshewa mkataba wake, na tatu kama kuna Klabu yeyote inayo muhitaji ije tufanye transfer” amesema Injinia Hersi Said
Feisal Salum hajaitumikia Young Africans tangu mwezi Desemba mwaka 2022, na alitegemea huenda angeihama klabu hiyo wakati wa Dirisha Dogo la Usajili, lakini hatua hiyo ilishindikana baada ya kuingia katika mgogoro wa kimkataba na waajiri wake.