Licha ya mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kuwa gumzo baada ya timu zilizotinga hatua hiyo kufahamika, Uongozi wa Azam FC umetoa kauli ya kupotezea.
Azam FC iliyotangulia Fainali baada ya kuichapa Simba SC 2-1 mjini Mtwara, itacheza dhidi ya Young Africans iliyoibanjua Singida Big Stars 1-0 mwishoni mwa juma lililopita.
Uongozi wa Azam FC umesema kwa sasa hawaifikirii Fainali ya michuano hiyo badala yake akili zao zipo kwenye michezo yao miwili ya mwisho ya ligi kuu Tanzania Bara ambapo wanataka kumaliza vizuri mechi hizo za mwisho msimu huu.
Azam FC kwenye ligi inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama 53 ikipishana kwa alama mbili dhidi ya Singida Big Stars yenye alama 51 wakivutana kumaliza katika nafasi hiyo.
Afisa Habari wa Azam FC, Thabiti Zakaria ‘Zaka’ amesema kuwa wanachokiangalia hivi sasa ni mechi zao mbili za ligi kuhakikisha wanaibuka na alama sita zilizobakia kwa kuwa fainali ya ASFC bado haijapangwa.
“Hii mechi ya ASFC bado hatujui itachezwa lini kwa sababu TFF bado hawajaipangia ratiba, hatuwezi kuifikiria kwa sasa, sisi tunaelekeza nguvu kwenye michezo yetu miwili ya mwisho kwenye ligi na baada ya hapo ndipo tutaanza mikakati kwa mchezo huo, wa fainali baada ya kufahamu. tarehe ya mchezo,” amesema Zaka
Amesema kujiandaa na michezo hiyo miwili ya mwisho, awali waliweka kambi lakini baada ya bodi ya ligi kupangua ratiba waliamua kuvunja kambi na kuwapa wachezaji wao mapumziko mafupi.
“Lakini kwa sasa wachezaji wamerejea kwenye mazoezi kujiandaa na michezo hii miwili, malengo yetu ni kuhakikisha tunamaliza vizuri ligi msimu huu kwa kusanya alama zote sita zilizosalia,” amesema Zaka
Bodi ya ligi imetangaza michezo ya mwisho kuhitimisha msimu huu wa ligi kuu itachezwa Juni 9.