Mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar, Salvatory Ntebe amesema Dickson Job ni bonge la beki kuwahi kumwona katika kizazi hiki na kwake msimu huu wa Ligi Kuu ndio mlinzi bora wa mashindano hayo ambayo kwa sasa yakiwa ukingoni kumalizika.
Ntebe amesema Job ni beki mtulivu sana na anayefanya kazi nzuri uwanjani isiyotumia nguvu na anatumia zaidi akili kitu ambacho walinzi wengi wanashindwa kufanya hivyo.
“Job ananivutia sana haswa akicheza beki wa kati anatumia akili sana kuliko nguvu pia ana utulivu mkubwa wakati anafanya majukumu yake ya kuzuia mashambulizi mabeki wa aina hii ni mara chache sana kuona anafanya faulo,”amesema Ntebe na kuongeza;
“Kwa sababu muda mwingi anakuwa anacheza 11 na mpira na sio mwili wa mtu hivyo anakuwa achezi rafu tofauti na mabeki wengine ambao wanatumia zaidi nguvu kuliko akili ndio maana wanacheza sana faulo kwangu Job ndio beki bora msimu huu Ligi Kuu.”
Beki huyo wa kati alisema alikiona mapema kipaji cha mchezaji huyo wakati anachezea kikosi cha vijana cha Mtibwa Sugar ambapo aliona Job atakuja kuwa staa mkubwa kutokana na kujituma kwake. Job yuko kwenye kikosi cha kwanza cha Young Africans na Taifa Stars kwa muda mrefu sasa.
“Wakati tupo Mtibwa Job alikuwa timu B niliona kipaji chake nilimwambia Vicent Barnabas ambaye ndio alikuwa kocha wao kuwa huyu dogo ni bonge la mchezaji na kama akiendelea kujituma atafika mbali sana na kweli leo amekuwa staa.”
“Alikuwa na juhudi sana mazoezini kikubwa nimwombe aendelee kujituma na kwangu nitafurahi siku moja kumwona akicheza soka la kulipwa ulaya kwani uwezo anao wa kucheza huko,” amesema Ntebe