Mbunifu wa jezi za Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Sheria Ngowi amesema jezi za klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa 2023/24 zipo tayari na kwa sasa wanasubiri michezo ya fainali umalizike ili uzinduzi wa jezi hizo ufanyike.
Ngowi amekuwa mbunifu wa Jezi za Young Africans kwa msimu wa pili mfululizo, huku wadau wengi wa Soka la Bongo wakimsifia kwa ubinifu wake, ambao huwavutia Mashabiki na Wanachama wengi wa klabu hiyo kununua jezi kwa wingi baada ya kuzinduliwa.
Akizungumza kupitia Shirika na Utangazaji la Tanzania ‘TBC’, Ngowi amesema baada ya kumaliza ubunifu wa Jezi za klabu ya Young Africans zitakazotumika msimu ujao, Uongozi wa klabu hiyo ulimwambia unasubiri kuchezwa kwa Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ili kufanya uzinduzi.
Amesema Jezi za msimu ujao za Young Africans zina ubora wa hali ya juu na rangi zake zinavutia, hivyo anaamini Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo wataendelea kuvaa jezi zilizo na ubora.
“Ubunifu tumeshaufanya na taratibu zote zimeshakamilika, kwa sasa Uongozi wa Young Africans unasubiri kumalizika kwa michezo ya Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, ili tufanye uzinduzi.”
“Jezi za Young Africans ubunifu wake ni wa hali ya juu, sioni wa kuifikia. Wabuni rangi tu” Amesema Ngowi.
Katika Hatua nyingine Sheria Ngowi ameushukuru Uongozi wa Young Africans kwa kuwa soko linazidi kukua huku akibainisha kuwa klabu nne za Afrika zimemfuata kutaka azitengenezee jezi huku mbili zikiwa za hapa Nchini.