Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema uteuzi wa Mels Daalder utakuwa na msaada mkubwa kwake katika mchakato wa kukisuka upya kikosi chake cha msimu ujao.
Mapema juma lililopita uongozi wa miamba hiyo ya soka nchini Tanzania, ulimtambulisha Mels kama Mkuu wa Idara ya kusaka vipaji (Skauti), ambaye atasaidiana na Benchi la Ufundi katika usajili wa dirisha kubwa kwa ajili ya msimu ujao.
Kocha huyo alieleza kuwa elimu na uzoefu aliokuwa nao Mels katika kutambua vipaji vyao wachezaji vitasaidia kupata wachezaji sahihi watakaosaidia timu hiyo kufikia malengo ambayo wamekusudia kuyafikia kuanzia msimu ujao.
“Ni mtu sahihi kwetu ujio wake utakuwa na faida nyingi kwa klabu ikiwemo kupata wachezaji wenye ubora stahiki kulingana na ukubwa wa Simba SC, naupongeza uongozi pamoja na Mohammed Dewji kwa hiki, naamini Simba ya msimu ujao itakuwa ya tofauti,” amesema Robertinho
Kocha huyo ameeleza kuwa amepanga kukutana na Mels ili kumsikiliza kipi alichopanga kuanza nacho na yeye kumpa aina za wachezaji anaowahitaji ili waweze kuanza mchakato huo mara moja sababu wanakabiliwa na michuano ya Super Ligi hivi karibuni.
Amesema katika kikosi chake cha msimu ujao amepanga kusajili wachezaji wasiopungua wanane wapya ambapo kati yao watano watakuwa wageni na watatu wazawa baadhi yao tayari wameanza mazungumzo nao na anafurahi kuona mambo yanakwenda vizuri.
Uongozi wa Simba SC umedhamiria kufanya mapinduzi makubwa kwenye usajili pamoja na kuliboresha benchi lao la ufundi ili kuwa na kikosi bora kitakacho irudisha timu hiyo kwenye ubora iliokuwa nao zamani.