Uongozi wa Simba SC umebainisha kuwa, utakuja kivingine ndani ya msimu mpya wa 2023/24 kwa kuleta wachezaji wenye sifa ya ushindani na kutafuta matokeo mazuri bila kukata tamaa.

Kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Simba SC imegotea nafasi ya pili, baada ya kucheza mechi 28 ina alama 67, wakiachwa na Young Africans iliyotwaa Ubingwa kwa kufikisha alama 74.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema watafanya kazi kubwa kwenye maboresho ya kikosi kwa kuwaongeza wachezaji wazuri watakaoleta ushindani.

“Huu haukuwa msimu mzuri kwetu, ambacho tunakifanya kwa sasa ni kuangalia pale ambapo tulikwama na kuboresha kikosi kwa ajili ya kupata matokeo mazuri kwenye mechi zetu msimu ujao.

“Yaliyotokea tumeona na kwa sasa tunafanyia kazi kwani mpira una mambo mengi yanatokea, na sisi tunazidi kujiimarisha kuwa kwenye mwendo mzuri utakaotufanya tuje kivingine,” amesema bosi huyo.

Wakati huo huo Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’, Kocha Mkuu wa Simba, amesema kuwa anahitaji maboresho zaidi kwenye kikosi hicho ili kuongeza ushindani ndani ya timu hiyo.

Kocha huyo raia wa Brazil, amesema Simba SC ini timu kubwa ambayo inajulikana kila kona ya dunia, hivyo ni muhimu kuwa na wachezaji wenye morali kubwa na ari ya upambanaji mwanzo mwisho.

Mbrazil huyo baada ya kuchukua mikoba ya Zoran Maki, kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, kaiongoza Simba SC katika mechi 9, akiambulia sare mbili dhidi ya Namungo na Azam FC zote ilikuwa kwa kufungana bao 1-1.

Robertinho amesema: “Kwenye eneo la wachezaji ni muhimu kufanya maboresho kwa kuwa na wachezaji wakubwa wenye uwezo, hii itakuwa sawa ndani ya kikosi kutokana na ukubwa wa Simba SC.

“Unajua Simba SC ni timu kubwa inajulikana, wa hata Brazil wanaizungumzia, sasa tukiwa na wachezaji wazuri na wenye uwezo itakuwa rahisi kutupa matokeo bora na kuleta ushindani.

“Tumekuwa na mwendo ambao umekuwa mzuri, lakini sio kwa kiasi kikubwa, hii ilitokana na kuwa na wachezaji ambao ni majeruhi na adhabu za kadi zimekuwa zikifanya tusiwatumie wachezaji wengine.”

Young Africans yalalamikiwa kufanya hujuma Kwa Mkapa
Mitungi ya Gesi ni salama - Makamba