Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans Injinia Hersi Said ametamba wana matumaini makubwa ya kupindua meza dhidi ya USM Alger, katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Young Africans baadae leo Jumamosi (Juni 03), itakua na kibarua kigumu cha kuikabili USM Alger katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa Fainali Kombe la Shirikisho mjini Algiers kwenye Uwanja wa 5 July 1962, huku ikiwa nyuma kwa mabao 2-1, yaliyofungwa kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa jijini Dar es salaam Jumapili (Mei 28).
Hersi Said amesema dharima kubwa ya kikosi cha Young Africans katika mchezo wa leo ni kupindua meza kama walivyofanya dhidi ya Club Africain ya Tunisia, baada ya kutoka sare ya bila kufungana jijini Dar es salaam na kisha walishinda ugenini 1-0.
“Tupo tayari kwa ajili ya mchezo huu muhimu, kama timu tunajua wapi tulipoteleza kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza na tayari tumefanya marekebisho na tunaamini huu utakuwa mchezo tofauti.
“Kuna baadhi ya watu wanadhani mchezo umeisha kwa kuwa tulipoteza mabao 2-1 nyumbani, lakini niwahakikishie kuwa tuna nafasi ya kuwashangaza watu kwa kupindua meza hapa Algeria kama ambavyo tulifanya dhidi ya Club Africain kule Tunisia.” Amesema Hersi
Kikosi, viongozi na baadhi ya Mashabiki wa Young Africans waliondoka nchini juzi Alhamisi (Juni Mosi) kwa ndege maalum iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.