Mabingwa wa Ujerumani FC Bayern Munich wanatarajia kuwapiga bei washambuliaji wake watatu kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi ikiwa ni mpango wa kukifumua kikosi hicho kwa ajili ya msimu ujao.
Bayern Munich walishinda ubingwa wa Bundesliga kwa mbinde msimu huu na hilo lilitokana na Borussia Dortmund kutoka sare na Mainz katika mchezo wa mwisho wa msimu.
Ndani ya msimu huo, Bayern ilimfuta kazi pia Kocha Julian Nagelsmann na kumteua Thomas Tuchel, huku ikiambulia patupu kwenye Kombe la Ujerumani na Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Na sasa, Bayern inaripotiwa ipo tayari kuwapiga bei mastaa wake watatu kwenye safu ya ushambuliaji, Leroy Sane, Sadio Mane na Serge Gnabry kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Mastaa hao wote watatu hawakuwa kwenye ubora mkubwa sana msimu huu na Bayern inataka wapambanaji kwa ajili ya kurudi na nguvu mpya msimu ujao.
Mastaa Mane na Sane waliripotiwa kugombana wenyewe kwa wenyewe kwenye vyumba vya kubadilishia nguo mchezo wao wa kichapo baada ya Manchester City kwenye Ligi kutoka ya Mabingwa Ulaya.
Mane aliripotiwa kumpiga ngumi ya mdomo Sane, jambo lililomfanya baadaye supastaa huyo wa zamani wa Liverpool, anayeitumikia Senegal kwenye soka la kimataifa kuomba radhi kwa kitendo la shambulio la mwilini alilofanya kwa mchezaji mwenzake.
Mane ameshindwa kuonyesha kiwango cha kutosha tangu alipotua Bayern Munich tofauti na alivyokuwa akikipiga Anfield chini ya Kocha Jurgen Klopp.