Benchi la ufundi la Azam FC linaloongozwa na Kocha Mkuu, Youssouph Dabo, limeutumia mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ili kukamilisha mikakati ya kuifunga Young Africans na hatimaye kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Azam FC itakutana na Young Africans katika mechi ya fainali ya Kombe la ASFC itakayochezwa Jumatatu (Juni 12), mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini, jijini Tanga,
Mkuu wa Kitengo cha Habari ya Azam FC, Thabit Zakaria amesema, Dabo na wasaidizi wake wameifuatilia Young Aficans katika michezo yake mikubwa mitano iliyopita na tayari amefahamu ‘njia’ watakazopita ili kupata matokeo mazuri watakapowavaa kwenye mechi ya fainali ya ASFC.
Zakaria amesema licha ya akili na nguvu za wachezaji wao kufikiria pia mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara zilizosalia, kocha wao anaijenga timu kila idara kuhakikisha wanamaliza msimu kwa furaha baada ya kushindwa kutwaa mataji mengine.
“Ni kweli kabla ya kukutana na Young Africans tuna mechi mbili za ligi, wachezaji wamepewa maagizo ya kusaka alama sita katika, mechi zetu hizo, ila hilo halimfanyi kocha wetu kutowafuatilia wapinzani wetu wa fainali ya ASFC.
Lazima ajue mbinu za kiufundi za mpinzani wake kabla ya kucheza fainali, kuna mechi tatu ambazo watacheza wiki hii, kuanzia jana zote ziko katika mipango yetu, mwalimu anawafatilia, atarudi na mbinu za kuwamaliza,” amesema Zakaria.
Kuhusu maandalizi ya mchezo dhidi ya Coastal Union, kiongozi huyo alisema kikosi chao kinaondoka Dar es Salaam leo kuelekea Tanga kuwafuata wenyeji Coastal Union kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa keshokutwa.
Ameongeza baada ya mechi hiyo watarejea Dar es salaam mapema ili kuwakaribisha Polisi Tanzania ambao watakutana nao kwenye mchezo ya kumaliza msimu.