Mshambuliaji nyota wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Young Africans Fiston Mayele, raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), amesema anatarajia kuweka wazi hatima yake ndani ya kikosi hicho hivi karibuni.
Mayele mwenye mabao 16 katika Ligi Kuu Tanzania Bara ndiye anaongoza katika orodha ya wafungaji na ni kinara wa kupachika mabao kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika iliyomalizika Jumamosi kwa Young Africans kushika nafasi ya pili.
Akizungumza jijini Dar es salaam kabla ya kuanza safari ya kuelekea jijini Mbeya kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko wa 29 wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City Mayele, amesema ataweka wazi timu ipi ataichezea katika msimu ujao baada ya kukamilisha uamuzi wake.
Mayele amesema huu ni msimu wake bora kufanya vizuri kwa kutwaa Tuzo ya Mfungaji Bora kwa Afrika na sasa anatarajia kutafuta Kiatu cha Dhahabu kwa upande wa Tanzania.
Mshambuliaji huyo amesema ni mapema kuweka wazi kwa sababu bado hawajamaliza msimu na mipango yake ni kuhakikisha Young Africans inafanya vizuri katika michezo miwili iliyosalia.
“Huu ni msimu mzuri, nimefanikiwa kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa Afrika, pia nina mechi mbili za ligi ninaimani nitafanya vizuri na kutwaa kiatu cha ufungaji bora.
Kuhusu mkataba wangu ni mapema sana kwa sababu bado msimu haujaisha na matarajio yangu kuwapa kipaumbele Young Africans kulingana na mahitaji yao ya msimu ujao,” amesema Mayele.
Ameongeza kukosa kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa msimu huu imetokana na kukosa bahati, lakini walijipanga kuwa mabingwa na ndio maana walipambana kila walipoingia Uwanjani.
“Haikuwa bahati yetu, licha ya kupata ushindi, tumehukumiwa na kanuni,” Mayele amesema.
Katika hatua nyingine Mayele amesema alipata maumivu kidogo mguuni katika mechi ya fainali na anatarajia kupata mapumziko ya siku mbili ambayo anaamini yatamweka fiti na kurejea vizuri kumalizika michezo miwili ya Ligi Kuu iliyosalia pamoja na fainali ya Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’.
Kwa upande wa Rais wa Young Africans Injinia Hersi Saidi, amesema wanatambua baadhi ya wachezaji wao muhimu akiwamo Mayele wako katika siku za mwisho za mikataba yao na tayari wameshaanza mazungumzo kwa ajili ya kuhakikisha wanawabakiza klabuni hapo.
Hersi amesema watatumia njia tatu’ ili kuhakikisha wanamshawishi mchezaji huyo kubakia Jangwani kwa kumwandalia mazingira mazuri katika mkataba wake au wanamuuza na kutafuta mtu sahihi’ atakayechukua nafasi yake.
“Tunajivunia mchezaji wetu kutakiwa na timu zote kubwa za Afrika, ingeshangaza tufanye vizuri halafu isiwe kocha wala mchezaji wetu kutakiwa na timu nyingine, kama ikitokea hilo tunahakikisha tunazungumza na mchezaji ili kumbakiza ndani ya kikosi kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi,” amesema Hersi.
Rais huyo ameongeza wachezaji wa Young Africans kutakiwa na timu nyingine ni sehemu ya mafanikio kwa sababu inadhihirisha wana kikosi imara.
“Viongozi tuko makini katika kuhakikisha tunawabakiza baadhi ya wachezaji wetu ambao mikataba yao iko ukingoni, usajili wetu huu tutachukua nyota wenye kiwango bora ambaye atakuja kuongeza kitu kwenye kikosi,” Hersi ameongeza.
Kuhusu mipango msimu ujao ujao katika mashindano ya kimataifa, amesema kiongozi huyo ya malengo yao ni kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kikosi cha Young Africans kiliondoka jijini Dar es Salaam jana Jumatatu (Juni 05) usiku na kuelekea Mbeya kwa ajili ya mechi yake ya Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City ambayo pia itatumika kama sherehe za kukabidhiwa kombe la ligi hiyo.