Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Zanzibar, Yasin Mgaza anayeichezea KMKM iliyotwaa ubingwa wa ligi ya visiwani humo amesema kwa aina ya viungo waliopo Ligi Kuu Bara, Simba SC na Young Africans ana uwezo wa kumaliza msimu katika moja ya klabu hizo akiwa na zaidi ya mabao 20.

Licha ya kuwa huu ni msimu wa kwanza kucheza Ligi Kuu Zanzibar, Mgaza mwenye umri wa miaka 19 aliyetoka Ligi ya Champioship Bara amekuwa mfungaji bora Zanzibar akiwa na mabao 17 katika mechi 25 alizocheza KMKM na asisti nane.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Mbuni FC amesema hayo baada ya kuvichambua vikosi vya Simba na Young Africans na kuona anaweza kufanya makubwa kwao.

“Ubora wa viungo wa Young Africans na Simba SC ni mkubwa. Wana wachezaji ambao wanaweza kuhimili presha ya mchezo wowote mkubwa,” amesema Mgaza.

“Tuliona uwezo wao hata kwenye michezo kimataifa. Binafsi kama nikipata nafasi kuwa sehemu ya kikosi mojawapo naweza kufunga zaidi ya mabao 20. Inawezekana watu hawanijui vizuri ila kwa ambao wamenifuatilia wameona kazi yangu na ndio maana zipo klabu za Bara zinataka kunisajili.”

Kabla ya kuondoka Mbuni FC msimu wa mwisho aliisaidia kupanda daraja, Mgaza alihusika kwenye mabao 22 akifunga 16 na asisti sita kwenye michezo 16.

Zipo taarifa Geita Gold, Mbeya City na Coastal Union ni kati ya timu za Bara zinazovutiwa na uwezo wa mshambuliaji huyo.

Majadiliano Tanzania, Dubai yalisimamiwa na Wataalam
Wanafunzi elimu ya juu wanalipwa Dola 154 kila mwezi