Mshambuliaji wa FC Lupopo ya DR Congo, George Mpole amesema kwa sasa anajifua vilivyo akifanya mazoezi mara mbili kwa siku kwa ajili ya kuwa sawa kuelekea msimu ujao.

Mpole ambaye hivi karibuni alisema anafikiria kutafuta timu mpya baada ya hali ya Ligi Kuu ya DR Congo kufutwa msimu huu na kwa sasa anajiweka sawa kwa ajili ya msimu ujao kama atajiunga na timu nyingine.

“Kipindi hiki cha mapumziko, ligi zinaenda mwishoni nimekuwa najipanga zaidi kwa ajili ya msimu ujao maana si mbali, kwa sasa nimekuwa nikifanya mazoezi mara mbili kwa siku, mfano asubuhi naenda ‘gym’ na jioni nafanya mazoezi mengine ya mpira, lengo ni kujiweka sawa zaidi,” amesema Mpole

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Geita Gold amesema hiyo ni program ambayo alipewa kutoka Lupopo, hivyo amekuwa akiitumia na inamuweka vizuri zaidi kwa ajili ya kuhakikisha msimu ujao anaendelea pale alipoishia.

Mpole amewahi kukipiga Real Nakonde ya Zambia, Mbeya City, Polisi Tanzania kabla ya kung’ara msimu uliopita akiwa na Geita akiibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara kwa kufunga mabao 17 kabla ya msimu huu kutimkia Lupopo.

Fursa, rasilimali zipo, Vijana wajiajiri - Makamu wa Rais
Young Africans waipa kongole Azam FC