Mshambuliaji kutoka nchini Uruguay Luis Suarez huenda akajiunga na wachezaji wenzake wa zamani wa FC Barcelona, Lionel Messi na Sergio Busquets kwenye klabu ya Inter Miami kwa mujibu wa ESPN.
Juma lililopita Lionel Messi alithibitisha kujiunga na Inter Miami msimu huu wa joto, ambapo ataungana na rafiki wa karibu Sergio Busquets.
Na sasa Suarez ambaye alikuwa karibu sana na Messi pale Camp Nou, pia atajiunga na kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya Marekani, MSL.
Messi anatua huko kwa uhamisho wa bure baada ya kumaliza mkataba wake na Paris Saint-Germain, na vile vile Busquets anakwenda bila malipo baada ya kuondoka Barcelona mwishoni mwa msimu wa Ulaya wa 2022/23.
Suarez amekuwa na klabu ya Gremio ya Brazil tangu mwaka jana baada ya kuitumikia klabu ya Nacional nchini kwao.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 36 ana mkataba na Gremio hadi mwaka 2024, lakini ana kifungu cha kutolewa ambacho yeye na Miami wameanzisha na usajili wake utathibitishwa hivi karibuni.
Kuwasili kwa Suarez kusini mwa Florida kutamaanisha kurejea kwenye kikosi sawa na Messi na Busquets kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2020, alipoondoka Camp Nou na kuelekea Atletico Madrid.
Watatu hao walikaa pamoja kwa miaka sita yenye mafanikio makubwa kule Katalunya na inaaminika kuwa Messi ametekeleza jukumu lake katika kusaidia kuwaleta wachezaji wenzake wa zamani kwenye klabu hiyo.