Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi amewashukuru wachezaji wake kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa msimu wa 2022/23, ambao rasmi ulifikia tamati jana Jumatatu (Juni 12).
Young Africans ilifunga rasmi msimu huo kwa kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ kwa kuichapa Azam FC 1-0, katika Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.
Nabi amesema shukrani zake zinakwenda kwa wachezaji wake, kwani umekuwa msimu wenye michezo mingi kutokana na kucheza mashindano yote iliyoshiriki hadi mwisho.
“Tusingeweza kufika safari hii ndefu bila hawa. Wamekuwa makini na mipango yote ya timu kuanzia mwanzo, tulikuwa na mchezo mgumu lakini vijana wamesimama katika maelekezo.
“Tangu juzi nilisema kuwa tuna timu ya kushindana, japo ukweli utabaki kuwa tuna uchovu, lakini haikuwa sababu kwani ilikuwa lazima tucheze mchezo huu,” amesema Nabi
Mbali na kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara, Young Africans pia imetwaa Ubingwa wa Ligi Kuu sambamba na kufika Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.