Aliyekuwa Beki na Nahodha wa Arsenal, Per Mertesacker, anaamini kuwa klabu hiyo ipo katika nafasi nzuri ya kumsajili Ilkay Gundogan kutoka Manchester City.

Gundogan mwenye miaka 32, amefanya kazi kubwa msimu wa 2022-23 na kuandika historia ndani ya Manchester City kwa kutwaa mataji matatu ‘treble’, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Premier League na FA.

Kiungo huyo mkataba wake na Man City unaisha Juni, mwaka huu na amekuwa akiwindwa na klabu kadhaa za Ulaya kama Arsenal, FC Barcelona na Borussia Dortmund, lakini kocha Pep Guardiola anataka kuona nahodha wake huyo anasalia ndani ya kikosi cha Man City.

Mertesacker ambaye kwa sasa ni kiongozi katika Akademi ya Arsenal, amesema: “Nafikiri klabu ipo katika nafasi nzuri. Najua (Mikel) Arteta anamfahamu vizuri na atakuwa na mawasiliano naye.

“Kwa sasa ngoja kwanza tumuache achague mwenyewe ni klabu gani kati ya nne ambayo atakubali kwenda.”

Baada ya kuwepo kwa tetesi nyingi, hivi karibuni, Gundogan alibainisha kwamba: “Bado sijafanya uamuzi juu ya hatma yangu, lakini muda si mrefu itafahamika.”

Vipimo, utafiti: Hakuna mgonjwa hata mmoja - Dkt. Kaniki
Robertinho ataka mtu zaidi ya Baleke