Naibu Waziri wa Maji, Mary-Prisca Mahundi amesema makisio ya bajeti ya Mpango wa Nchi wa WaterAid (2023-2028) ni shilingi bilioni 45.87 ambapo kuna ongezeko la shilingi bilioni 9.07 ikilinganishwa na mpango uliopita.
Mahundi ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa Mpango wa Nchi wa WaterAid (2023-2028) na maadhimisho ya miaka 40 ya Shirika la WaterAid Tanzania, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Amesema, fedha zilizotengwa kwenye mpango mpya zitatumika kuboresha sekta ya maji katika maeneo ya huduma endelevu, jumuishi na salama ili kuleta mabadiliko makubwa. “Nitumie fursa hii kuwapongeza WaterAid Tanzania kwa kutekeleza mpango wao uliopita.”
Naibu Waziri huyo, pia amewashukuru wadau wote wa maendeleo wanaochangia katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya sekta ya maji kwa kuwa michango yao ya kifedha na kitaaluma ni muhimu katika kuendeleza na kuboresha utoaji huduma.
Awali, Mkurugenzi Mkaazi wa WaterAid Tanzania, Anna Mzinga alisema shirika hilo katika kipindi cha miaka 40 tangu lianze kazi nchini, limeweza kushirikiana na Serikali kuwafikishia huduma za maji watu milioni nane, ambapo watu 800,000 walipatiwa vyoo bora na watu milioni 26 walihamasishwa masuala ya usafi wa mazingira wanayofanyia kazi katika mikoa 11 ya Tanzania Bara na Zanzibar.