Wababe wa Kaskazini mwa jijini London Arsenal wana nafasi kubwa ya kumsajili Kiungo Declan Rice kutoka West Ham United kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku klabu hizo zikijapanga kuanza mazungumzo juu ya ada inayopaswa kulipwa.

Rice mwenye umri wa miaka 24, pengine ameshacheza mechi yake ya mwisho kwenye kikosi cha West Ham United wiki iliyopita wakati alipoisaidia timu yake kushinda ubingwa wa Europa Conference League kwa kuichapa Fiorentina katika mchezo wa fainali na kuwa timu ya kwanza ya England kubeba taji hilo.

Baada ya kuzungumzwa sana kwa miezi hii michache iliyopita juu ya hatima ya kiungo huyo katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya na sasa inaonekana atabaki jijini London.

Kwa mujibu wa The Guardian, Arsenal imeweka mazingira mazuri ya kumnyakua Rice kutokana na chama hilo kufikia hatua nzuri kwenye makubaliano ya ada ya uhamisho na wenzao West Ham.

Arsenal ipo tayari kulipa ada ya awali ya Pauni 90 milioni kwa ajili ya kunasa saini ya kiungo huyo, huku ada yake ya jumla inaweza kufikia Pauni 100 milioni kutokana na nyongeza nyingine.

Kocha Arteta anaamini kwa kuinasa saini ya Rice itamuwezesha kutengeneza kikosi cha ushindani kitakachoweza kuchuana na timu imara kama Manchester City katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao 2023/24.

RC Mwassa ataka maboresho ushindani soko la Kahawa
Onana aikamua Simba SC Milioni 189.5