Hii leo, Tanzania inaungana na nchi zingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, ambalo ni azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika – OAU, mwaka 1990, baada ya mauaji ya kinyama ya watoto wa kitongoji cha SOWETO nchini Afrika ya kusini na serikali ya Makaburu Juni 16, 1976.

Watoto hao, walikuwa wakidai haki zao za kutobaguliwa pamoja na haki nyingine za kibinadamu ikiwemo haki ya kupata elimu bora na hivyo kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi ambapo baada ya tukio hili, OAU iliazimia kuwa tarehe 16 Juni ya kila mwaka iwe Siku ya Mtoto wa Afrika.

Siku ya tukio, waliandamana zaidi ya nusu maili wakidai pia haki ya kufundishwa kwa lugha yao, ambapo watoto zaidi ya 100 waliuwa na askari Polisi wa utawala wa makaburu wa Afrika ya Kusini wakati huo.

Kufuatia mauaji hayo, na kwa kutambua umuhimu na thamani ya watoto ndipo azimio la nchi 52 wanachama wa uliokuwa Umoja wa nchi huru za Afrika (Organization of African Unity – OAU), kwasasa African Unity – AU ndipo waliipitisha tarehe hii ya 16 Juni ya kila mwaka, kuwa ni siku ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.

Hivyo basi, Tanzania kama zilivyo nchi nyingine mwanachama wa Umoja wa Afrika, imekuwa ikiadhimisha siku hii tangu mwaka 1991, ikiongozwa na kauli mbiu mbalimbali ambazo zimekuwa zikibeba ujumbe wa maadhimisho katika mwaka husika.

Kupitia maadhimisho haya, inatufanya tutathmini utekelezaji wa Sera za Taifa zinazohusu maendeleo ya watoto kwa kuwapatia huduma stahiki ikiwa ni pamoja na afya, elimu, ulinzi na malezi bora ili kuwarithisha stadi mbalimbali na tunu za kitaifa kwa manufaa yao, familia na Taifa la Tanzania.

Kauli mbiu katika Maadhimisho ya 2023 ni “Zingatia Usalama wa Mtoto katika Ulimwengu wa Kidijitali” ikielekeza watoto, wazazi na wanajamii kuchukua hatua za kutetea haki za watoto zilizoainishwa katika Sera ya Mtoto (2008), ambazo ni Haki ya Kuishi, Kuendelezwa, Kulindwa, Kushiriki na Haki ya Kutobaguliwa kwa namna yoyote akiwa nyumbani, shuleni au kwenye jamii.

DAR24 tunaungana na Tanzania, Afrika na wote wenye mapenzi mema na watoto Duniani bila kubagua rangi, dini wala kabila tukisema “Mtoto ni msingi wa Taifa Endelevu: Tumtunze, Tumlinde na Kumuendeleza.

Sote kwa pamoja, tunakumbushwa kuandaa mipango thabiti ya kuwaendeleza watoto na kukuza ufahamu wa wazazi, walezi na jamii kuhusu kuzitafutia ufumbuzi na utatuzi wa changamoto zinazowakabili watoto wa Tanzania na Afrika kiujumla. 

Mume alalama kunyimwa unyumba, kupigwa na mkewe
Ally Kamwe: Mayele huenda akaondoka