Wakati Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans ikithibitisha kuachana na Kocha Nasreddine Nabi, Uongozi wa Klabu hiyo una majina matano ya makocha wanaopewa kipaumbele cha kukabidhiwa  Benchi la ufundi klabuni hapo.

Majina hayo matano ya Makocha wenye wasifu mkubwa katika Bara la Afrika, ymepatikana baada ya Young Africans kuanza mchakato wa kumsaka mrithi wa Nabi, ambaye anadaiwa kuwa katika hatua za mwisho za kumalizana na Uongozi wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

Taarifa kutoka ndani ya Young Africans zinaeleza kuwa majina ambayo yapo mezani ni matano hadi sasa na wote wanachagizwa na na rekodi nzuri katika soka la Afrika.

Kwenye majina hayo matano ni mmoja tu ambaye bado ana mkataba na timu aliyopo kwa sasa, wengine hawana timu, hivyo itakuwa rahisi kwa Young Africans kuwapata kirahisi.

Imefahamika kuwa majina ambayo yamefika mezani ni ya Pitso Mosimane mwenye miaka 58, Florent Ibenge (61), Juan Carlos Garrido (54), Faouzi Benzarti (73), Nabil Maaloul (60) na Omar Najhi.

Mosimane inaweza kuwa ngumu licha ya kuwa na urafiki na viongozi wa Young Afrucans, kwani mshahara aliokuwa akilipwa na Al Hilal ya Saudi Arabia ni Dola 100,000 (Sh230 milioni), ambao ni mkubwa zaidi.

Katika makocha hao, wanaopewa vipaumbele ni Waarabu Faouzi Benzarti na Nabil Maaloul, ambao wote ni raia wa Tunisia alipotokea Nabi.

Ibenge ni Kocha mwingine anayetarajiwa kutokana na urafiki wake na Rais wa Young Africans, Muhandisi Hersi Said.

Nabil, ambaye alikuwa Kocha wa Esperance ya nchini Tunisia alinyanyua ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo mara tatu, misimu ya 2010/11, 2011/12 na 2021/2022.

Upande wa kimataifa, Nabil alitwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) msimu wa 2010/11 akiwa na Esperance na msimu uliopita alikwenda nchini Kuwait akiwa na klabu ya Kuwait SC na alibeba ubingwa wa Ligi Kuu 2021/22.

Kwa upande wa Faouzi, ambaye anakinoa kikosi cha Es Sahel (Étoile Sportive du Sahel) kinachoshiriki Ligi Kuu Tunisia na yupo kwenye orodha hii na mkataba wake na timu hiyo unamalizika Juni 30, mwaka huu.

Faouzi, ambaye anatumia mfumo wa 4-2-3-1, ametwaa ubingwa wa Tunisia mara tisa akiwa na timu tofauti za Esperance, Etoile du Sahel na Club Africain.

Faouzi pia alibeba Kombe la Ligi Tunisia 2014/15 akiwa na Etoile du Sahel. Kwenye Ligi ya Morocco ametwaa ubingwa misimu miwili mfululizo akiwa na Wydad Casablanca 2018/19 na 2020/21.

Kimataifa ametwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 1993/94 akiwa na Esperance Tunis na Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2014/15.

Jina lingine kubwa ni kocha raia wa Morocco na England, Omar Najhi, ambaye amewahi kuifundisha Wydad Athletic ya nchini humo akiwa kama kocha msaidizi.

Najhi mwenye umri wa miaka 45, ana leseni ya ukocha ya juu ya UEFA Pro akiwa na ile ya CAF A, mbali na kufanya kazi Wydad, msimu wa 2021/22 alikuwa kocha wa klabu ya Mouloudia Oujda iliyoshiriki Ligi Kuu Morocco.

Mwigulu: Simba SC ifuate nyayo za Young Africans
Magugu maji ziwa Victoria yaundiwa mkakati