Baada ya ya Kocha Nassredine Nabi kuondoka baada ya kumaliza mkataba wake Young Africans, sasa ni zamu ya kiungo mkabaji, Yannick Bangala ambaye inaelezwa kuwa yupo mbioni kuondoka kwenda katika timu hiyo.
Kocha Nabi anatajwa kwenda kujiunga na klabu ya Kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini mara baada ya kumaliza mkataba wake Young Africans.
Chanzo cha kuaminika ambacho ni rafiki wa Bangala kutoka DR Congo kimefichua siri hiyo, ambayo huenda ikawashtua mashabiki na wanachama wa Young Africans.
Rafiki huyo amesema kuwa, kiungo huyo ana ofa nyingi mezani kwake na baadhi ya klabu zimeonyesha wazi kuwa tayari kuvunja mkataba ndani ya Young Africans na kumbeba kiungo huyo ambaye ni mchezji bora wa ligi kuu msimu uliopita.
Kiliongeza kuwa, kati ya ofa hizo kuna klabu moja kutoka Tanzania na nyingine ni za nje ya nchi hivyo uwezekano wa kubaki Young Africans ni 20% pekee na 80% ni za kuondoka.
“Bangala ana ofa nyingi sana ambazo zipo mbele yake, katika ofa hizo zote kuna timu kubwa sana ambazo zimeonyesha nia ya kweli ya kuhakikisha kuwa wanampata mchezaji huyo ambaye ni mmoja kati ya wachezaji walioonyesha mafanikio makubwa ndani ya Young Africans.
“Bangala mwenyewe yupo tayari kuondoka ndani ya Young Africans kutokana na kukosa nafasi ya kucheza katika michezo ya mwisho na yeye mwenyewe yupo tayari kwenda kutafuta changamoto mpya mara baada ya kufanya vyema akiwa na Young Africans kwa kuipatia makombe yote muhimu,” kimeeleza Chanzo hiko.
Alipotafutwa Bangala ili azungumzie ishu hii amesema: “Ni kweli mimi nina ofa kubwa kutoka nje ya Tanzania na timu nyingine kubwa kutoka hapa hapa Tanzania zimeonyesha nia ya kunitaka, kwangu nimebakiza mkataba wa mwaka mmoja kuendelea kuichezea Young Africans hivyo niseme kuwa nina asilimia 20 za kubaki Young Africans na nina asilimia 80 za kuondoka.”