Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba SC, Amri Said ‘Jap Stam’ amesema aliyekuwa Kocha Mkuu wa Young Africans, Nasreddinne Nabi ameacha somo kubwa katika soka la Tanzania, huku akiwafundisha makocha wazawa kujiamini.
Nabi raia wa Tunisia, ambaye alifahamika kwa misimamo yake bila kukubali kuingiliwa kwenye majukumu yake, Young Africans ilitangaza kuachana naye Juni 14, baada ya kumaliza mkataba wake akidumu kwa miaka miwili na nusu.
Akiwa na Young Africans, Kocha huyo alifanikiwa kutwaa mara mbili mfululizo mataji mawili ya Ligi Kuu, Ngao ya Jamii na Kombe la FA (ASFC) na kufika Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku akiweka rekodi ya kucheza mechi 49 bila kupoteza.
Stam, ambaye aliwahi kuzinoa Mbao FC, Biashara United na Lipuli FC, kwa sasa ni kocha wa KVZ ya Zanzibar, alimtaja Nabi kama mtu aliyewafundisha mambo mengi makocha wengine.
“Sisi kama makocha tumejifunza kwanza kocha unatakiwa kujiamini, pia falsafa yake timu yake inacheza mpira tu pasi fupi na za chini chini na hata wachezaji pia aliowafundisha kuna vitu watakuwa wamejifunza kwake,” amesema Stam
Mbali na Nabi, Stam aliwataja makocha wazawa, Fikirini Elias wa Coastal Union, Fredy Felix ‘Minziro’ (Geita Gold) na Denis Kitambi wa Namungo FC kuwa wamefanya vizuri msimu huu katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kuhusu tetesi za kurudi Bara, Stam amefunguka kuwa bado yupo sana Zanzibar katika klabu yake ya KVZ, kwani ana malengo makubwa ya kuisaidia klabu hiyo, huku akiweka wazi kuwa bado hakuna timu za Bara zilizomtafuta.