Siku moja baada ya aliyekuwa Msemaji wa Young Africans Haji Sunday Ramadhan Manara kuonekana katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliohusu Tamasha la SAMAKIBA, Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ limetoa tamko la kuwakumbusha wadau wa soka kutojihusisha na waliofungiwa kujihusisha na soka.
Manara anatumikia kifungo cha miaka miwili, baada ya kukutwa na hatia ya utovu wa nidhamu dhidi ya Rais wa TFF Wallace Karia, lakini uwepo wake katika Mkutano huo, ni dhahir umekuwa sababu ya tamko hilo ya ‘TFF’.
Katika taarifa ya TFF iliyotolewa mapema leo, imesisitiza kufuatilia ukiukaji huo ili kuchukua hatua stahiki.
Taarifa hiyo imeeleza: Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawakumbusha wanafamilia ya mpira wa miguu kuwa ni kosa kushirikiana na wadau ambao wamefungiwa.
Ni muhimu kuzingatia kuwa wadau husika wamefungiwa baada ya kwenda kinyume na Katiba, Kanuni na taratibu zinazosimamia mpira wa miguu.
Hivyo, TFF inaendelea kufuatilia ukiukaji huo ili kuchukua hatua stahiki.
Wanafamilia wote wanao wajibu wa kuheshimu Katiba, kanuni na taratibu zinazotawala mpira wa miguu.
Pia waliofungiwa wanajiweka katika hatari ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu iwapo hawatatumikia adhabu zao kikamilifu.