Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umesema hatima ya aliyekuwa Kocha msaidizi klabuni hapo Cedric Kaze, itafahamika mara baada ya kupatikana kwa Kocha Mkuu, huku pia ikiweka wazi kila kitu kuhusu Yannick Bangala na Tuisila Kisinda ndani ya kikosi hicho.

Afisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema kwa sasa wapo kwenye mchakato wa kumpata Kocha Mkuu na atakapokabidhiwa majukumu ndiye atakayeamua kuendelea kufanya kazi na benchi lililopo akiwamo Kaze, au kuja na watu wake.

Kutokana na hali hiyo, hatima ya Kocha huyo raia wa Burundi kubaki Young Africans au kuondoka, itategemea maamuzi ya Kocha Mkuu atakayekuja.

“Sasa hivi mazungumzo yaliyopo ni kumpata Kocha Mkuu, tukishampaka ndiyo tunampa fursa ya kuchagua wasaidizi wake, akitoa ruhusa tutaendelea na mazungumzo, yeye ndiye atakayetuambia watu gani anaotaka kufanya nao kazi kwenye Benchi lake la Ufundi.

“Akisema anawahitaji sawa, lakini anaweza kusema anakuja na Benchi lake la Ufundi, ndiyo dunia ya mpira wa sasa ilipofikia na sisi Young Africans ni weledi,” amesema Kamwe

Akizungumzia juu ya taarifa za mchezaji wao Bangala kutaka kuondoka, amesema kwa sasa ni mchezaji wa Young Africans aliyebakisha mwaka mmoja lakini kama akipata ofa nono, yenye maslahi kwa pande zote mbili klabu haiwezi kumzuia.

“Mpaka sasa ana mkataba wa mwaka mmoja, na mwaka wake uliobakia tunapitia ripoti ya Benchi la Ufundi tukisubiri kumpata Kocha Mkuu mpya, lakini tunaongea na mchezaji mwenyewe, halafu hatima yake itatolewa.

Apata ofa, klabu ikasikiliza kama inakuwa na maslahi ya pande zote basi itamruhusu, lakini mpaka tunavyozungumza Bangala bado ni mchezaji halali wa Young Africans,” amesema

Kuhusu kuachana na Tuisila Kisinda, Kamwe amesema amemaliza mkataba wake wa mkopo wa mwaka mmoja kutoka Klabu ya RS Berkane na sasa anarejea huko.

Chongolo aendelea kusikiliza changamoto za Wananchi
2023/24: 12 kutemwa Coastal Union