Tume ya Mpango wa Taifa, imeshauriwa kuandaa dira mahsusi yenye muelekeo wa kesho na mipango ya muda mrefu, ili kila awamu ya Urais inayoingia madarakani iweze kutimiza lengo kusudiwa, kwa manufaa ya nchi na Wananchi.

Rai hiyo imetolewa na Mbunge Kawe, Josephat Gwajima wakati akifanya mahojiano na Dar24 Media hivi karibuni na ameongeza kuwa watu hawahitaji rais mwenye maoni bali yule ambaye ataweza kutimiza maono ya Taifa ambayo aliyakuta tayari yamepangwa.

Amesema, “Rais ni muajiriwa na yupo pale kutimiza maono ya Waajiri wake (Wananchi), nchi za kiafrika rais huyu anaingia anakwenda kushoto, anaingia mwingine anakwenda kulia anaingia mwingine anakwenda mashariki, sasa kwa mfumo huo huwezi kuwa na maendeleo kama hakuna maono ya nchi.”

Mbunge Kawe, Josephat Gwajima.

Aidha, Gwajima ameongeza kuwa, “kwa mfano tunaweza kusema ndani ya miaka 30 kila mtanzania awe na nyumba ya bati, maji safi na salama, kila barabara iwe ya lami, kila Wilaya iwe na Chuo Kikuu cha Serikali na Hospitali ya rufaa na ndani ya muda huo yote yatimie, hapo tunakuwa tumetimiza maono kusudiwa.”

Hata hivyo, amesema mipango ya muda mrefu itasaidia vijana wanaokwenda chuo kuchagua wasome nini kwasababu wanajua ndani ya miaka 30 kutakuwa na soko la namna gani kwa kulenga fani mbalimbali zilizopo ndani ya dira ya Taifa.

Kocha Namungo FC afichua usajili 2023/24
Msuva: Sina mpango wa kucheza Tanzania