Baada ya kukamilisha mpango wa kurejea Celtic Park kama Mkuu wa Benchi la Ufundi, Brendan Rodgers amefichua kuwa alipopigiwa simu na mabosi wa Celtic kuhusu kupewa kazi ya kuinoa timu hiyo hakujiuliza mara mbili ili kufanya maamuzi.
Rodgers ambaye aliwaporomosha daraja Leicester City, sasa ubwabwa wake atakuwa anakula Celtic ya Scotland kwa mkataba wa miaka mitatu.
Rogers alikuwa na Celtic baada ya kuachana na Liverpool miaka kadhaa nyuma na kufanikiwa kutawala soka la Scotland na kuifanya Celtic kuwa tishio.
Lakini alipopata dili la kurejea tena England akawaacha Celtic kwenye mataa na mashabiki wakiwa wanahitaji zaidi uwepo wake kwenye klabu hiyo.
Akizungumza baada kutambulishwa kuwa kocha mkuu wa Celtic akichukua mikoba ya Ange Postecoglou aliyepata kibarua Tottenham, Rodgers amesema atahakikisha anashirikiana na mabosi na mashabiki kuhakikisha timu hiyo inakuwa moto wa kuotea mbali.
“Nimefurahi sana kurudi Celtic na nimefurahishwa sana na nafasi hii nzuri. Nilipopewa fursa ya kuombwa kujiunga na klabu tena, ulikuwa uamuzi rahisi sana kwangu na kwa familia yangu.
“Ange amefanya kazi nzuri katika miaka miwili iliyopita na nitafanya kila niwezalo kudumisha kasi ya Celtic kwenye mashindano ya ndani na ya Ulaya.
“Klabu iko katika hali nzuri kwenye ngazi zote na ningependa kuishukuru bodi kwa kuweka imani yao kwangu ili kuipeleka timu mbele.
Tutashirikiana kwa karibu sana tunapojitahidi kuleta mafanikio hayo kwa mashabiki wetu,” amesema Rodgers.