Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira ‘Robertinho’ amesema jumla ya wachezaji watatu tayari usajili wao umekamilika na kilichobaki ni kuwatambulisha.

Wachezaji wanaotajwa kumalizana na Simba SC hadi sasa na kupewa mikataba ya miaka miwili ni Mfungaji Bora wa Rwanda, Willy Onana anayekipiga Rayon Sports na mshambuliaji wa Vipers SC ya nchini Uganda, Milton Karisa.

Zipo taarifa nyingine zikihiusisha Simba SC kuwaleta wachezaji wa kigeni zaidi ya wawili ambao waliletwa kwa ajili ya kukamilisha usajili wao.

Akizungumza kutoka nchini Brazil Robertinho amesema, kuna wachezaji watatu waliosajiliwa ambao wote wapo katika mipango yake baada ya kukabidhi ripoti ya usajili kwa uongozi.

Robertinho amesema kuwa amefurahishwa na jambo hilo ambalo wamelifanya uongozi kwa kuwasajili wachezaji waliokuwepo katika mipango yake msimu ujao.

Ameongeza kuwa, anaamini msimu ujao, watafanya vizuri ikiwemo kubeba mataji yote wanayoyashindania ya ndani, pia kucheza Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Hadi sasa tayari kuna wachezaji kama watatu waliosajiliwa na wote ni sehemu ya mipango yangu baada ya kuwakabidhi ripoti viongozi wangu.

“Nimefurahishwa kwa jambo hili, naamini hadi kumalizika kwa orodha niliyoitoa kwenye ripoti yangu nitakuwa na timu bora na imara itakayoleta ushindani mkubwa msimu ujao.

“Niwashukuru viongozi wangu, hiyo imenipa matumaini makubwa ya sisi kufanya vizuri, ninaamini nitafanya kazi yangu vizuri katika msimu ujao,” amesema Robertinho.

Son Heung-Min akataa ofa Saudi Arabia
Hakuna wa kukuondolea changamoto, pambana - Kasesela