Aliyekuwa Kocha wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi ameondoka Dar es salaam na kama kuna mtu anayetamani kusepa naye atakapomalizana na klabu mpya basi ni Kocha wa Viungo, Helmy Gueldich aliyefanya naye kazi kwa ufanisi, hata hivyo huenda dili lisiwepo tena kwa kutosana.

Nabi aliyeinoa Young Africans kwa miaka miwili na nusu na kuwapa jumla ya mataji saba pamoja na kuifikisha Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, amekuwa akihusishwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, lakini wapinzani wakuu wa AmaKhosi, yaani Orlando Pirates wameanza hesabu za kumbeba fundi huyo wa mazoezi mwenye elimu ngazi ya Profesa ya mazoezi ya kisasa.

Amakhosi wanataka kumchukua Nabi akawe kocha wao mkuu, lakini sharti kubwa walilopewa na Kocha huyo ni kwamba anataka atue hapo na wasaidizi wawili na mmoja akiwa ni Helmy ambaye mashabiki wa Young Africans wanamkubali sana kwa mazoezi na mzuka wake anapokuwa kazini.

Hata hivyo, Orlando wameamua kutimia mkono kwenye dili hili wakitaka kumchukua haraka Helmy ili akaimarishe benchi la ufundi la timu hiyo, hususani kitengo cha mazoezi ya viungo ya wachezaji wakivutiwa na ufanisi wake alipokuwa Young Africans.

Akili hiyo ya Orlando inatokana na kunusa hesabu ndefu za watani wao Amakhosi ambao walikuwa wakivuatana na Kocha wa viungo wa sasa Muzi Maluleke ambaye bado alikuwa na mkataba na klabu hiyo.

Helmy mkataba wake na Young Africans unafikia mwishoni mwezi huu, huku mashabiki wa klabu hiyo wakiwa hawataki kusikia habari za kocha huyo atimke klabuni, lakini Wasauzi wamempania.

Imefahamika kuwa Nabi amemkataa Maluleke raia wa Afrika Kusini akidai sio mtaalamu mwenye mazoezi ya kisasa kwa wachezaji wa soka, hivyo anapambana Amakhosi kumuingiza Helmy kwenye Benchi lake jipya.

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa Helmy ambaye tayari yuko kwao Tunisia zinasema atalazimika kusubiri kujua muelekeo wa Nabi kutua Amakhosi, ambapo endapo dili hilo litakwama atafanya maamuzi mengine ikiwa ni kama kumtosa, kusudi maisha yaendelee.

Kocha huyo wa Viungo amekuwa maarufu kwa mashabiki kutokana na midadi ya ushangiliaji wa mabao ya Young Africans, ambapo huwa wa kwanza kuungana na wachezaji uwanjani kushangilia kila bao likifungwa tofauti na watu wengine wa Benchi la Ufundi la timu hiyo iliyotwaa mataji kibao wakiwa na Nabi.

Msuva azitega Simba, Azam FC, Young Africans
Nyoni aibukia Lindi, Gadiel Michael atemwa