Kwa mujibu wa Kamusi ya Kiswahili fasaha, inatuma maana ya neno Mjinga kuwa ni mtu asiyejua au kufahamu, ingawa wengi wa watu huchanganya neno mjinga na mpumbavu maana upumbavu ni ile hali ya mwanadamu kufanya jambo isivyotakiwa, huku akiwa na kuelewa namna ya kufanya inavyotakiwa.

Kuna kipindi ambacho marehemu Mzee Jongo (Msanii nguli wa Maigizo), aliwahi kusema, “kusoma sio kuufuta ujinga, bali ni kuupunguza,” hii inamaanisha kuwa kila mwanadamu ana ujinga wake maana kuwa na ujinga wa jambo sio kosa, kwani hata Profesa anaweza asijue nini afanye ili utokee Ugali halafu kijana wa miaka kumi akawa ni hodari wa ‘kutoa kitu’ (kupika ugali).

Lakini jambo hili, pia liliwahi kutolewa ufafanuzi na Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere akisema, “mjinga akishaambiwa inakwisha, kwasababu ujinga ni kutojua maana hujui inafanyika nini kwahiyo ukielezwa inakwisha, lakini upumbavu ni kipaji kama ufupi na urefu.”

Umati juu ya Gari ndogo ikipita kituo cha ukaguzi cha Ufaransa huko Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Desemba 16, 2013. Picha ya Jerome Late/ AP.

Nimeona nianze kwa kuandika hayo kwasababu Duniani kuna mambo mengi ya kushangaza na hayaishi kiasi watu hujiuliza ili kupata jawabu je? huu ni ujinga ama upumbavu….. nitakupa visa vichache halafu kupitia tafsiri za hapo juu bila kujali matumizi ya neno ujinga ama upumbavu nawe waweza kuwa hakimu.

Ipo hivi…… mwaka 2015 idara ya huduma za dharura nchini Marekani yenyewe ilimtangaza mkazi mmoja kuwa mjinga kuliko wajinga wote duniani baada ya jamaa huyo kupiga simu za kijinga katika idara hiyo akilalamika kuwa zipu ya koti la mkewe haifunguki.

Baada ya kupokea simu hizo za mara kadhaa mfanyakazi wa idara hiyo ya dharura alishangazwa na kauli ya mkazi huyo na kumuuliza kama mkewe anashindwa kupumua vizuri kwa tukio hilo lakini jamaa akajibu ya kwamba anapumua vizuri tu ila tatizo ni koti lake halivuki.

Idara hiyo ilimshauri mkazi akate hiyo zipu lakini akakataa na kusisitiza apelekewe wafanyakazi wa huduma za dharura wakamsaidie mkewe na ilibidi mfanyakazi wa idara hiyo afike kumsadia na ndipo baada ya kisa hicho jamaa akatunukiwa tuzo ya mtu mjinga zaidi duniani.

Kisa cha pili ni Mwizi ambaye aliwatumia polisi picha nzuri ili waitumie katika tangazo la kutafutwa kwake akisema ile waliyoisambaza ni mbaya na haifai, ambapo Polisi walikuwa wakimuhitaji kwa tuhuma za kuteketeza na kuharibu mali.

Anaitwa, Donald “Chip” Pugh, anasema alipoiona picha iliyotumiwa na Polisi alifadhaika ikabidi apige ‘Selfie’ na kuwatumia maafisa wa polisi huku akiandika ujumbe unaosomeka, “Hii hapa picha yangu nzuri, hiyo mliyotumia ni mbaya sana.”

Picha ya kushoto ndiyo iliyokuwa imetumiwa na polisi yeye aliwatumia iliyo kulia.

Polise hao katika mji wa Lima, jimbo la Ohio, walikuwa wamepakia picha kwenye ukurasa wao wa Facebook wakiomba msaada wa kumtafuta Pugh walibaki wameduwaa na hata hivyo walimjibu kuwa angefanya hisani zaidi kwa kujipeleka kwao ili ajisalimishe lakini hakufanya hivyo hadi pale alipokamatwa baadaye jimbo la Florida.

Funga kazi ya kujua kama huu ni ujinga ama upumbavu ni ya tukio la Gaidi aliyejitokeza kudai zawadi na kuwacha Maafisa wa usalama wa nchini Afghanisan vinywa wazi kwa mshangao baada ya kamanda huyo wa kundi la Taliban kujisalimisha na kisha kutaka apewe zawadi ya Dola 100 iliyokuwa imeahidiwa kwa mtu ambaye angesaidia kukamatwa kwake.

‘Mwamb’a anaitwa Mohammad Ashan, alikuwa anatuhumiwa kupanga mashambulio dhidi ya wanajeshi wa Marekani na Afghanistan mashariki mwa nchi hiyo na ripoti zinasema alifika katika kizuizi cha polisi mwaka 2012, akaelekeza mkono wake kwenye bango lenye picha yake na kisha akadai zawadi hiyo ya $100.

Maafisa wa usalama walishangaa sana na kushindwa kuelezea kitendo chake ambapo Afisa mmoja wa Marekani anadaiwa kuawaambia wanahabari kwamba, “kusema kweli mwanamume huyu ni mpumbavu,” kazi kwako msomaji kutoa hukumu juu ya visa hivi je? ni UJINGA au UPUMBAVU.

CAF Super League kubatizwa jina jipya
Huduma ya dharula afya ya akili ni muhimu - Kamati