Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal Pape Ousamane Sakho huenda akaondoka Simba SC katika kipindi hiki cha Dirisha la Usajili kuelekea msimu ujao 2023/24.
Sakho amekuwa akihusishwa na taarifa za kutaka kuondoka klabuni hapo tangu msimu uliopita, lakini mkataba uliopo kati yake na Simba SC umekuwa kikwazo.
Taarifa kutoka nchini kwao Senegal zinaeleza kuwa, Kiungo huyo anawindwa na klabu ya K.V.C. Westerlo inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ubelgiji, ambayo ipo tayari kuzungumza na Uongozi wa Simba SC katika kipindi hiki.
Klabu hiyo inadaiwa kuandaa Ofa ya Dola za Marekani 500,000 (Zaidi ya bilioni 1.1 za Kitanzania), ili kufanikisha usajili wa Sakho kutoka Mitaa ya Msimbazi yalipo Maskani Makuu ya Simba SC.
Hata hivyo kama Ofa hiyo itawasilishwa Simba SC, uongozi wa klabu hiyo utakuwa na kila sababu za kuikataa ama kuikubali, kutokana na thamani ya Sakho ambaye alisajiliwa klabuni hapo miaka miwili iliyopita akitokea kwao Senegal katika klabu ya Teungueth FC.
Pape Sakho bado ana mkataba na Simba SC ambao utafikia kikomo mwishoni mwa msimu ujao 2023/24.