Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuboresha na kuimarisha mifumo ya kieletroniki katika ukusanyaji wa mapato, mazingira ya kufanyia kazi kwa ujenzi wa Ofisi za kisasa, upatikanaji wa vitendea kazi na utoaji wa mafunzo kwa watumishi ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia mahitaji yaliyopo.

Dkt. Mwinyi ameyasema hayo hii leo Juni 24, 2023 katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma Zanzibar na kuzindua mifumo mitatu ya kieletroniki ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-Wakil na kuongeza kuwa Serikali pia italinda na kuimarisha maslahi ya wafanyakazi.

Amesema, “Serikali itaziimarisha Taasisi zote zinazoshughulika na usimamizi wa utawala bora ikiwemo ZAECA, CAG, DPP na Tume ya maadili kwa Viongozi wa umma kwa kuzipatia nyenzo na mafunzo ili ziweze kusimamia kwa ufanisi zaidi masuala yanayohusu uwajibikaji, uadilifu, uwazi, upatikanaji wa haki na huduma bora kwa wananchi na kutunga sheria mpya zinazohitajika ili kuzipa nguvu zaidi taasisi hizo.”

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ametoa wito kwa watumishi wote kuitumia mifumo yote iliyoanzishwa ili kuleta tija iliyokusudiwa na kuimarisha ufanisi katika Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi pia ameuhimiza uongozi wa wakala wa Serikali mtandao uongeze kasi katika kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma.

Tangu Serikali ya Awamu ya Nane ilipoingia madarakani, jumla ya mifumo 28 ya kieletroniki imetengenezwa kwa kuongeza ufanisi katika uwajibikaji na utoaji wa huduma bora na mitatu imezinduliwa rasmi leo ikiwa ni pamoja na jumuishi wa taarifa za watumishi na malipo utakaorahisisha mwenendo wa miamala ya fedha na kudhibiti wizi.

Baba Neymar mikononi mwa Polisi Brazil
Hofu ya Nketiah yaziita West Ham, Crystal Palace, Fulham