Beki kutoka nchini Kenya, Joash Onyango ameiweka Simba SC pabaya baada ya kukomaa kuondoka kwa kuandika barua kwa uongozi, huku mabosi wakimchomolea kutokana na kutokuwa na uhakika wa kumpata mbadala wake hadi sasa mbadala.

Onyango aliyesajiliwa na Simba, Agosti 2020 kwa mkataba wa miaka miwili kisha kuongeza mmoja msimu uliopita unaomalizika katikati ya msimu ujao, ameomba kuondoka akidai kutokuwa na furaha klabuni tangu msimu uliopita.

Hata hivyo, hadi sasa mabosi wanaendelea kujadiliana, huku wengi wakimzuia asiondoke kwanza hadi wapate mbadala na kama itashindikana atamalizia mkataba alionao kabla ya kuruhusiwa dirisha dogo litakalofunguliwa katikati ya Desemba, mwaka huu.

Habari kutoka ndani ya Simba SC zilizothibitishwa na mmoja wa mabosi aliyeomba kuhifadhiwa jina aliyesema wanahaha kupata mbadala wake atakayekuwa mhimili kwenye safu ya ulinzi ila hajapatikana.

Inaelezwa, endapo hawatapata beki imara kama Onyango au kumzidi wataendelea naye hadi mkataba utakapomalizika, kwani hawapo tayari kuona mabeki wa kati wawili akiwamo Mohamed Ouattara wanaondoka kwenye kikosi.

“Msimamo wa Onyango bado ni uleule wa kutaka kuondoka, ila hawezi kuruhusiwa kama hatutapata beki mwingine mzuri, hivyo atasubiri hadi dirisha dogo ila akipatikana ataachwa kama alivyoomba,” kimesema chanzo hicho.

Ugumu wa kumzuia Onyango unaelezwa ni kutokana na mabosi kushindwa kupata mbadala ambapo wameanza usajili wa chinichini wakisubiri dirisha la usajili lifunguliwe Julai Mosi hadi Agosti 30, japo hadi sasa wamesajili nyota Mcameroon Leandre Onana.

Mbali na Onana ambaye ni winga aliyekuwa Rayon Sports ya Rwanza, Simba inampigia hesabu kipa Mbrazil Caique Luiz Santos da Purificacao na Mrundi Fabien Mutombola pamoja na Alfred Mudekereza waliopo Vipers waliopendekeza na kocha Roberto Oliveira.

Hata hivyo inaelezwa makipa wawili wa Vipers huenda wakapigwa chini na kubakishwa Mbrazili ambaye atakayeungana na kipa Ally Salim wakati Aishi Manula anasubiriwa kurejea kutoka majeruhi, huku fagio la kuwaacha karibu wachezaji 12 ambao hawahitajiki kwa sasa kikosini.

Fagio hilo limeanza na mastaa wanane hadi jana wakati tunakwenda mitamboni.

Chanzo: Mwanaspoti

Mkude afunguka ishu ya Young Africans
Unai Simon: Benzema alisumbua sana La Liga