Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mstaafu, Philip Mangula amewataka Vijana nchini kupenda kujisomea na kujibidiisha katika safari zao kisiasa, akisema uongozi unahitaji kujituma na kujitolea na pia ni wito wa kuijua siasa na si kujua kuongoza, kwani kuongoza watu ni karama na hivyo ni vyema kuandaa misingi kuanzia ngazi ya shina na waelewe kuwa mafanikio mwenzake ni changamoto.
Mangula ameyasema hayo wakati akifanya mahojiano na Dar24 Media nyumbani kwake jijini Dodoma hivi karibuni, na kuongeza kuwa kwa sasa dunia imekuwa ni kijiji lakini hiyo haifanyi mtu ashindwe kujibidiisha katika utafutaji wa maarifa, hivyo ni vyema wakajiwekea utaratibu ambao utakuja kuwafaa katika maisha yao ya baadaye.
Amesema, “ili ufanikiwe tenga muda wa kutosha kuishughulisha akili na nafsi yako kuyafikiria na kuyachakata mambo yako kwa utulivu, kwasababu huko ndiko kwenye vyanzo vyote vya nguvu za hatua zako katika kuielekea hatma yako, lakini haya yote uyafanye huku ukiwa na fikra kwamba mafanikio pacha wake ni changamoto, zipo changamoto.”
Philip Japhet Mangula, ‘Mzee wa Mafaili’ ni kiongozi wa enzi za uongozi wa kofia mbili ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera (1993-1996), na wakati huohuo akiwa ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Mkoa akiwa na historia ndefu ndani ya CCM na siasa kiujumla, Mwandishi wa habari, kada na kiongozi wa CCM kwa ngazi mbalimbali.