Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema endapo Madini yasiposimamaiwa vizuri na mamlaka husika yanaweza kusababisha migogoro ya kisiasa kwani mali za asili mara nyingi hugeuka kuwa laana ya nchi kwa wahusika kukesha kutafuta rasilimali hizo ili kujikomboa kiuchumi.
Waziri Biteko ameyasema hayo wakati akizungumza na Dar24 Media na kuogeza kuwa ni makosa makubwa kuamini tumeshafika wakati tunapaswa kwenda mbele zaidi na kwamba uongozi madhubuti unaosimamia vizuri mgawanyo sawa na kwa haki utaondoa malalamiko na kuepusha migogoro.
Amesema, “Watanzania wanatamani tufanye vizuri zaidi katika sekta ya madini, kitu kinachofanya wakati wote tujiangalie ili tupunguze umasikini, tunazo rasilimali nyingi hasa nchi zetu za Afrika, tumezungukwa na utajiri mkubwa wa asili ambao hatujawekeza chochote, Mungu ametupa lakini kwa kiwango kikubwa haujabadilisha maisha ya waafrika.”
Biteko ameongeza kuwa, Tanzania imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha Madini yanawanufaisha Watanzania kupitia na awamu zote ikiwemo ya kwanza iliyosema kutokujipanga kunasababisha shughuli za uchimbaji wa madini zisubiri ili yachimbwe baadaye.
“Awamu zingine zilizofuata zilitunga sheria na baadaye kuona sheria zina matobo mengi, tukarekebisha tukagundua kanuni haziwabebi watu wetu, hazitusaidii kukuza uchumi na kwamba tunayo madini ni lazima yatubadilishie maisha yetu,” amesema Waziri Biteko.
Hata hivyo, amesema bado Taifa la Tanzania halijaingia katika migogo ya madini kutokana na utamaduni uliopo akibainisha kuwa mazingira ya kisiasa ni mazuri na mtanzania yeyote anaruhusiwa kwenda kokote kuchimba au kuvuna rasilimali ili mradi awe amefuata sheria za nchi.