Mtu mmoja, Usman Buda mfanyakazi katika soko la machinjo katika wilaya ya Gwandu ya jimbo la Sokoto nchini Nigeria, amepigwa mawe hadi kufa baada ya kutuhumiwa kukufuru Dini ya Kiislam na Mtume Muhammad wakati wa ugomvi wake na mfanyabiashara mwingine sokoni
Kwa mujibu wa taarifa ya msemaji wa Polisi, Ahmad Rufa’i alisema tukio hilo limetokea eneo la kaskazini magharibi mwa nchi hiyo huku mamlaka na wanaharakati wakikemea jambo hilo lililozusha hasira kwa makundi mengine ya haki za binadamu yanayohofia vitisho vinavyoongezeka juu ya uhuru wa kidini katika eneo hilo.
Wakazi walisambaza video zilizoonekana kutoka eneo la tukio zikionyesha umati mkubwa wa watu ambao ulijumuisha watoto wakimrushia mawe Buda, ambaye alikuwa Kalala sakafuni huku wakimlaani na Rufa’i alisema kikosi cha polisi kilipelekwa katika eneo hilo lakini walipofika, kundi hilo lilikimbia na kumuacha mwathiriwa akiwa amepoteza fahamu na alifariki baadaye katika hospitali ya Usmanu Danfodiyo huko Sokoto.
Mauaji hayo ni mashambulizi ya hivi karibuni ambayo wanaharakati wa haki za binadamu wamesema yanatishia uhuru wa kidini katika eneo la kaskazini mwa Nigeria lenye Waislamu wengi na yakiwa yamebeba adhabu ya kifo chini ya sheria ya Ki-islamu katika eneo hilo.