Wakili wa rais wa zamani wa Zambia, Edgar Lungu amelaani hatua ya serikali ya nchi hiyo kutwaa mali mbalimbali, zinazohusishwa na familia mwanasiasa huyo na kusema kuwa kitendo hicho kimechochewa kisiasa kufuatia Rais wa sasa wa Zambia, Hakainde Hichilema kukabiliana na ufisadi.
Mlalamiko hayo yanakuja baada ya Serikali kutwaa rasmi mali hizo kutoka kwa familia ya Lungu wiki jana, ambazo ni pamoja majengo 15 ya orofa mbili mbili, nyumba ya kulala wageni ya orofa tatu, shamba na nyumba ya kawaida ambazo zimechukuliwa kwa mujibu wa Sheria ya Utaifishaji wa Mapato ya Uhalifu ya mwaka 2010,yanayoruhusu Serikali kutwaa mali ambayo inaamini ilipatikana isivyo halali.
Wakili wa Rais huyo wa zamani, Makebi Zulu amesema yeye wala wateja wake hawajapewa notisi ya mchakato wowote ulio mbele ya Mahakama yoyote kuhusu kukamatwa kwa mali hiyo na hivyo wametoa maelezo ya kutosha jinsi walivyopata mali hizo na Serikali inazuia kwa makusudi taarifa hizo, ili kuwaaibisha Lungu, mke wake Esther Lungu, na watoto wao.
Wakosoaji wa Rais Hakainde Hichilema, wanasema tangu serikali yake ilipoanza kuwakamatwa viongozi wa utawala uliopita na kuwafanyia uchunguzi wa madai ya vitendo vya rushwa, hakuna yeyote kati yao aliyepatikana na hatia.