Mashabiki na Wanachama wa Simba SC wamepewa ufafanuzi wa kina kuhusu kimya kilichotawala katika klabu yao, baada ya juma lililopita kutembea kwa ‘Thank You’ kwa wachezaji ambao hawatakuwa sehemu ya kikosi msimu ujao 2023/24.
Mbali na wachezaji kuachwa, Simba SC ilitangaza kuachana na baadhi ya watendaji wa Benchi la Ufundi la Klabu hiyo, ambao nafasi zao zitajazwa na watendaji wapya watakaotangazwa siku kadhaa zijazo.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kimya kilichotawala kwa sasa ni kwa sababu wapo kwenye mazungumzo na baadhi ya wachezaji watakaotolewa kwa mkopo pamoja na wale ambao wanataka kuvunja nao mikataba.
“Hatujamaliza, ila kimya ambacho kimeonekana wiki hii ni kwa sababu tumemaliza wachezaji ambao tumewaacha, hatutokuwa nao msimu ujao na wamemaliza mikataba yao, lakini awamu ya pili itafuata kwa wachezaji ambao tutawatoa kwa mkopo kwenda klabu zingine, kwa sasa tupo nao katika mazungumzo, huwezi kutoa tu hivi hivi bila kumshirikisha.
Tukishakubaliana nao, basi mtaona tu tena taarifa zetu za mfululizo kuwa fulani tumempeleka kwa mkopo,” amesema Ahmed.
Mbali na hilo, amesema wapo wachezaji ambao klabu inataka kuachana nao, lakini bado wana mkataba, nao pia wako kwenye mazungumzo nao ili waachane kwa usalama na amani.
“Kuna Wachezaji ambao wana mikataba, lakini klabu haitaki kuendelea nao, tuko nao kwenye mazungumzo ya mambo ikiwamo mbalimbali, kuwalipa fidia na yakimalizika nao pia tutawaweka hadharani kama wale wa kwanza,” amesema.
Ahmed ambaye amerejea ofisini baada ya kupumzika kwa siku kadhaa kutokana na msiba wa baba yake mzazi, amesema wakishamaliza wachezaji wote, kitakachofuata ni kutambulisha watu wapya wa benchi la ufundi, kabla ya kutangaza wachezaji wapya.
“Tukimalizana nao, tutakuja na watu wa benchi la ufundi na baada ya hapo tutaanza sasa kushusha vyuma kimoja baada ya kingine,” amesema.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinasema wachezaji Joash Onyago na Ismael Sawadogo ni kati ya wachezaji ambao Simba SC inataka kuachana nao, lakini bado wana mkataba, hivyo mazungumzo bado yanaendelea.