Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umesema umempa jukumu zima la usajili Kocha Mkuu mpya Miguel Angel Gamondi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo Andre Ntine, kupitia tathmini ya ripoti ya kocha aliyepita kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha msimu wa 2023/24.
Young Africans ilimtambulisha Gamondi kuchukuwa nafasi ya Nasreddine Nabi, ambaye ameachana rasmi na kikosi hicho baada ya kupata ofa ya kuinoa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Afisa Habari wa Young Africans Ally Kamwe, amesema wako makini katika usajili wa wachezaji wapya kwa kumshirikisha Kocha Mkuu mpya Miguel Angel Gamondi kwa kufuata matakwa ya timu yao kuelekea msimu ujao wa mashindano.
“Bahati tuliyopata ni kocha mwenye uzoefu mkubwa wa soka la Afrika, viongozi wamezingatia falsafa ya Gamondi kwa kuboresha kikosi chetu, hakuna mchezaji wa Young Africans aliyesajiliwa kwa Chupli Chupli’,” amesema Kamwe.
Amesema usajili unafanywa kwa kuangalia ripoti ya mwalimu aliyepita Nabi ambayo imekabidhiwa kwa mkurugenzi wao wa ufundi na sasa watashirikiana vizuri na kocha Gamondi ili kuona ni aina gani ya wachezaji watakaosajiliwa.
“Tumefanya usajili mzuri, wachezaji tunaowaleta wanajua mpira, tumeshusha watu wa ukweli kulingana na mahitaji yetu ya msimu ujao kuendelea tulipoishia msimu huu iwe kutetea mataji yetu yote na kuleta Kombe la Afrika katika ardhi ya Tanzania,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa wamefanya usajili mkubwa na kusisitiza kuwa mchezaji atakayekuja kuvaa jezi namba sita ni balaa kwa kuwa anajua mpira na amefanya vizuri katika klabu aliyotoka.