Imefahamika kuwa Beki wa Pembeni wa Singida Fountain Gate FC, Nickson Kibabage amepewa mkataba wa miaka miwilina Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans.

Kibabange ambaye alifanya vizuri katika Ligi Kuu Bara msimu uliopita awali alikuwa akitajwa kuwa anaweza kujiunga na Simba SC, lakini jana Jumatano (Juni 28) ilifahamika kuwa amepewa mkataba wa miaka miwili na Young Africans na wamekubaliana atasaini Julai Mosi dirisha la usajili litakapofunguliwa.

Beki huyo wa kulia na kushoto amekuwa akizunguka na mkataba kwenye gari lake kusubiri tarehe rasmi ili asaini na kuwa mali ya Young Africans baada ya timu hizo mbili kuafikiana.

“Alipewa mkataba kuanzia wikiendi (iliyopita) akaenda akausoma na wakakubaliana kuwa upo sawa na hata fedha nyingine ameshapewa anatamba nazo mjini.

“Young Africans walikuwa wanataka kumsajili tangu dirisha dogo, lakini wakaachana naye,” kilisema chanzo kutoka Young Africans, licha ya beki huyo mahiri kusema bado usajili huo haujakamilika.

“Nimeziona taarifa hizo zinazosambaa mitandaoni, lakini ukweli mpaka sasa bado sijui kitu chochote labda Young Africans wanitake siku mbili hizi, lakini bado nina mkataba na Singida na lazima waanzie kwao,” amesema beki huyo aliyefunga mabao manne msimu uliomalizika.

Mbali na kucheza kama beki, Kibabage pia amekuwa akitumika kama winga kwenye baadhi ya michezo tangu akiwa Mtibwa Sugar na ni rasmi sasa ataungana na mastaa wengine aliocheza nao kwa mafanikio Mtibwa Sugar, kipa Abutwalib Mshery na mabeki Kibwana Shomari na Dickson Job.

Kabla ya kujiunga na Singida kwenye dirisha dogo, beki huyo aliwahi kukipiga Mtibwa Sugar, KMC na Difaa Al Jadida ya Morocco.

Inonga: 2022/23 ulikuwa msimu mgumu sana
Bangala, Djuma Shaban wabanwa Young Africans