Klabu ya Namungo FC imedhamiria kurudi tena kimataifa msimu ujao kwa kuhakikisha inamaliza Ligi Kuu katika nafasi ya juu kama ilivyo msimu wa 2019/20, ilipomaliza ya nne.
Katibu mkuu wa timu hiyo, Ally Suleiman amesema msimu wa kwanza kupanda Ligi Kuu walishiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika, lakini baada ya hapo hawakupata tena nafasi ya kumaliza nafasi nne za juu.
Katika misimu minne ya ligi Namungo imemaliza ya nne mara moja, tano mara mbili 2021/22 na 2022/23, huku 2020/21 ikimaliza nafasi ya tisa.
“Kambi tunatarajia kuianza mapema kwa maandalizi ya msimu ujao sababu lengo ni kumaliza nafasi za juu ili kushiriki kimataifa,” amesema.
“Julai 10 ndio siku ya kukutana wote jijini Dar es salaam ambapo tutaanzia kambi kwa muda kisha tutakwenda Zambia ili kuweka mambo sawa kulingana na kile ambacho tumelenga kwa ajili ya kukipata msimu ujao.”
Kuhusu kuimarisha kikosi, amesema hawatakuwa na mabadiliko makubwa sababu wachezaji wengi waliachwa dirisha dogo la Januari na wengine kuongezwa.
Amesema hawataongeza wachezaji zaidi ya watano wala kuacha wengi, huku akieleza usajili wa Erasto Nyoni lilikuwa pendekezo la kocha kutokana na udhaifu eneo la kiungo.
“Nyoni tulikuwa na malengo naye muda mrefu maana timu ilikuwa ina shida eneo la kiungo, hivyo kocha alishauri kama tunaweza kumpata mchezaji huyo na mwisho wa siku tulifanikiwa kumpata,” amesema.
Amesisitiza kuwa wachezaji watakaoachwa watatangazwa Jumamosi ya juma hili ili wapate muda wa kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.
Namungo ilianza msimu ikiwa chini ya kocha Honour Janza baadae ikamnasa Denis Kitambi.