Wakati Simba SC ikiachana na Kiungo Mundamizi Jonas Mkude, uongozi wa klabu hiyo umeamua kuvunja benki na kumpa mkataba wa miaka miwili kiungo aliyekuwa amewagomea, Sadio Kanoute.

Kanoute ambaye ameitumikia Simba SC kwa misimu miwili akitokea nchini kwao Mali amekubali kumwaga wino tena kwa miaka mingine miwili.

Chanzo cha taarifa kinasema awali Kanoute alitaka kuongezewa mshahara kutoka dola 8,000 (takriban Sh 19 milioni) hadi 10,000 (zaidi ya Sh23 milioni), jambo ambalo Simba SC waliona ni gumu, lakini wamejadili na kuamua kumpa mkataba.

Hata hivyo, inaelezwa Jumanne (Juni 27) walikubaliana na mchezaji huyo na kuamua kusaini miaka miwili akiwa nchini kwao, Mali.

“Kanoute alitaja pesa ambayo haikutarajiwa. Sasa ilibidi apewe kazi Mels Daalder ambaye ni skauti mkuu ili azipitie kazi za mchezaji huyo kama atafaa kuisaidia klabu ndipo waanze kufanya makubaliano naye na naona kila kitu kimekwisha,” kimesema chanzo.

Chanzo hicho kimesema kuwa staa huyo ameongeza mkataba kuitumikia timu hiyo hadi 2025.

Mbali na Kanoute timu hiyo pia imemuongezea mkataba Mshambuliaji Kibu Denis ambaye pia ataendelea kuwepo Msimbazi kwa miaka miwili.

“Kibu na Kanoute wote wataendelea kuitumikia Simba kwa miaka miwili. Ilikuwa sio rahisi kuwabakiza kutokana na kuwa miongoni mwa majina ya mapendekezo ya kocha.

“Bado zoezi la kuacha wachezaji na kuboresha timu linaendelea, hii ni kutokana na kufuata ripoti ya kocha. Kuna baadhi ya wachezaji tunaendelea na mazungumzo nao kwa ajili ya kuvunja mikataba na wengine kuwabakiza, hivyo muda wowote taarifa zitatoka,” kimesema chanzo hicho.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally amelizungumzia hilo kwa kusema: “Ripoti ya kocha imeonyesha wachezaji wanaowataka, hivyo viongozi wanapambana na wachezaji ambao wanataka kubaki nao kwa ajili ya kupambania taji la ligi ambalo tumelikosa misimu miwili mfululizo.”

Jurrien Timber awekewa mkakati Arsenal
Nilimpiga Polisi kumfundisha adabu - Mtuhumiwa