Beki wa pembeni kutoka DR Congo Joyce Lomalisa Mutambala amekubali kubaki kuendelea kukipiga katika klabu hiyo hadi msimu ujao 2024/25.
Hiyo ikiwa ni siku chache tangu beki huyo kipenzi cha Young Africans kutishia kuondoka klabuni hapo na kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.
Beki huyo alitishia kuandika barua ya kusitisha mkataba wake wa mwaka mmoja uliobaki huku akihusishwa kutakiwa Azam FC.
Taarifa kutoka Young Africans zinaleza, beki huyo alikutana na viongozi wa timu hiyo, kwa ajili ya kufanya kikao kizito na kufikia muafaka wa kubakia hapo.
Mtoa taarifa huyo amesema kuwa, katika makubaliano hayo beki ametoa sharti la kumalizia msimu wake wa mwisho kabla ya mazungumzo mengine kufanyika ya kubaki kukipiga hapo.
Ameongeza kuwa beki amekubali kutoa ushirikiano kwa benchi jipa la ufundi la timu hiyo, litakalokuwa chini ya Muargentina, Miguel Gamondi.
“Ishu ya Lomalisa na Young Africans imemalizika baada ya viongozi kufanya naye kikao juzi Jumatano na kufikia muafaka mzuri wa pande zote mbili za kubakia hapo.
“Hivyo katika kikao hicho Lomalisa amekubali kutoa ushirikiano mkubwa kwa benchi jipya la ufundi.
“Lomalisa ametoa ahadi ya kuipambania timu katika mashindano yote watakayocheza msimu ujao,” amesema mtoa taarifa huyo.
Lomalisa kupitia ukurasa wake wa kijamii alithibitisha kubakia Young Africans kwa kusema kuwa: “Nipo tayari kuipambania timu katika msimu ujao.”