Uongozi wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans umesema hatima ya kiungo, Jonas Mkude kwenye usajili wa timu hiyo msimu ujao 2023/24 iko chini ya kocha wao mpya Angel Miguel Gamondi.

Young Africans inatajwa kumalizana na Mkude ambaye hivi karibuni aliachwa na klabu yake ya Simba SC aliyoitumikia tangu mwaka 2010.

Tangu kuelezwa kuwa Young Africans inataka kumsajili kiungo huyo mkongwe wa Simba SC kumekuwa na maoni tofauti miongoni mwa wadau wa soka nchini.

Hata hivyo Afisa Habari wa Young Africans Ali Kamwe amesema, Mkude ni mchezaji mzuri na kila mmoja anafahamu juu ya uwezo wake ingawa amesema kocha wao Gamondi ndiye anashikilia hatima ya usajili wa nyota huyo kwenye klabu yao.

“Mkude ni mchezaji mzuri hakuna ambaye hajui uwezo wake, ni moja ya viungo wazuri tulionao nchini, naamini kwa uzoefu alionao anaweza kuwa na mchango wake kwa timu yoyote atakayokwenda, hakuna timu Tanzania inayoweza kubeza uwezo wake.

“Kwa hiyo kama itakuwa mipango ya Young Africans na uongozi kwa kushirikiana na kocha (Gamondi) wakiona inafaa, tutamkaribisha na naamini wanachama watakuwa na furaha kufanya kazi na kuona mtu mwenye uzoefu anaongezeka kwenye timu yetu,” amesema Kamwe.

Ingawa Mkude mwenyewe hajaeleza atatua wapi lakini Azam na Singida Fountain Gate pia zimekuwa zikitajwa kumuwania kwa ajili ya uzoefu alionao ndani ya ligi na michuano ya klabu Afrika.

Tata Martino afunguka safari ya Marekani
Usajili 2023/24: KMC FC yaongeza Milioni 300