Imefahamika kuwa Nahodha na Kiungo wa Polisi Tanzania, Tariq Simba anakaribia kumalizana na timu ya Kitayorce (Tabora United) kwa ajili ya kuitumikia msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

Kitayorce ya mkoani Tabora, itacheza Ligi Kuu msimu ujao mara baada ya kufanya vizuri katika Championship iliyomalizika hivi karibuni na kupanda pamoja na JKT Tanzania na Mashujaa FC ya Kigoma.

Simba, ambaye humudu kucheza nafasi za kiungo na beki wa kushoto amewahi kuzichezea klabu za Biashara na Tunduru Korosho.

Hata hivyo Kocha wa Kitayorce (Tabora United), Henry Mkanwa amesema bado hawajaanza kufanya usajili na muda ukifika wataweka wazi wachezaji watakaowasajili.

Kwa upande wa Simba amesema kwa sasa yupo tayari kucheza timu yoyote ambayo watakubaliana nayo kwa faida ya pande zote mbili.

“Mimi ni mchezaji, maisha yangu yanategemea soka nipo tayari kucheza timu yoyote, lakini kwa sasa sitaki kuweka mambo hadharani kwanza, subiri dirisha la usajili,” amesema kwa kifupi.

Mmoja wa marafiki wa mchezaji huyo, ambaye hakutaka jina lake litajwe hadharani amesema tayari Simba amesaini kandarasi ya mwaka mmoja kuichezea Kitayorce (Tabora United).

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Julai 2, 2023
Young Africans yaahidi kishindo juma lijalo