Kiungo Mshambuliaji Singida Fountain Gate, Ibrahim Ajibu ameeleza kuwa kinachowafanya wachezaji washindwe kung’ara wanaposajiliwa na timu kubwa za Simba SC na Young Africans ni uoga na kutojiamini kwenye kupambana.

Ajibu ameeleza hayo baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kufunguliwa kwa dirisha la usajili juzi Jumamosi (Julai Mosi) mpaka Agosti 31, mwaka huu.

Kiungo huyo aliyewahi kuwika akiwa Simba SC na Young Africans kwa nyakati tofauti, amesema kinachowavuruga wachezaji wa timu ndogo ni kukutana na wachezaji wenye uzoefu mkubwa wanapotua kwenye klabu kubwa na kongwe nchini, kitu ambacho mara nyingi humaliza ari walizonazo na kuonekana wamefeli.

“Unajua mchezaji akiwa timu ndogo au ya kawaida anaweza kuonekana lakini anapochukuliwa na kwenda timu kubwa changamoto huwa ni uzoefu wa watu anaokutana nao kikosini na kuingiwa woga, sasa kama wataacha uoga na kuanza kupambana wanaweza kucheza na kuwika,” amesema Ajibu.

Amesema anafahamu ni rundo la wachezaji wengi wazuri wanaishia njiani wanaposajiliwa na timu kubwa lakini hiyo yote inaweza kuzuilika kama mchezaji atajiamini na kuzizingatia ndoto zake kupitia soka na kipaji alichonacho na si kingine.

Zungumzeni, maneno ni tiba - Akina mama
Rais Samia atengua, ateua Wakuu wa Wilaya